FOODS



                                   TABORA , ASILI YA VIAZI


Na Cheupe Nyati




Viazi vitamu  vyenye rangi mbali mbali vikiwa vimepangwa kwa ajili ya mauzo Sokoni (Angalia kwa ukaribu utaona kuna aina nne hapo juu) Fungu la mwisho kulia ni tamu kuliko vile aina zingine.


Mkoa wa Tabora bado ni mingoni mwa mikoa iliyo mikubwa. Pamoja na ukubwa  wa eneo lake, jina la Tabora limeanzia mahali padogo sana. Jina hilo limeanzia katika kishamba kilicho kuwa kidogo ambacho kilikuwa kimetayarishwa kwa kuzalisha viazi.

Viazi kwa watu wa Tabora ni chakula ambacho ni kizuri sana na  kinapendwa na kina heshima kubwa. Viazi kwa lugha ya  watu wa mahali hapa vina majina mengi na tunaweza kutaja baadhi tu. Mkoa wa Tabora  tangu na tangu kulijulikana kuwa ni nyumbani kwa  Wanyamwezi ambao walikuwa  wametokea katika matumbo tisa[1].

 Majina yake viazi ni kama vile kafuu, shilumbu na vilumbu, na mengine yapo mengi.

Mji wa Tabora hivi sasa umepanuka sana na sehemu zilizopata umashuhuri ni kama vile kule Ipuli, Cheyo na Lwanzali. Sehemu zote hizo wakati nchi hii inapata Uhuru mwaka 1961, zilikuwa ni maeneo ambayo yako mbali na mjini. Bendera ya Uhuru ilipandishwa na watu waliishuhudia Union Jack ikishuka katika eneo ambalo linaitwa Kwa Manoli. Kote huko kume kuwa ni sehemua ya mji ambapo hapo ilikuwa ni kiwanja cha ndege cha zamani. 
Na Huko Ipuli, ambao ndio mji mpya sasa ilikuwa  ni mashamba tupu na kulijaa miembe tele. Kwa Tabora, kwa mambo ya Kihistoria, hukuona mtu kama kalima shamba  na akapanda mazao yake halafu asitie viazi. Walifanya hivyo kwa uzuri na Faida ya mmea huo.
Mmea huu ambao unajulikana kwa jina la  Kigeni kama Impomea Batatas, unatumika kwa Mnyamwezi  kuanzia mizizi, shina na hata mauwa na majani yake. Mashina ya mmea huu ambao hutambaa  huweza kutumika kama kamba kwa mtu ambaye anataka kufunga mizigo yake. Kina mama wakienda kuchanja kuni mwituni si ajabu wakachukua mashina ya viazi na kuyatumia kufungia kuni zao. Lakini mashina hayo  hutoa majani ambayo ni laini sana  na majani hutumika kama mboga za majani. Na utayarishaji wa mboga hizi uko namna kwa namna; kuna matumizi ya moja kwa moja na matumizi ya muda mrefu.
Matumizi ya moja kwa moja huchumwa Matembele (majani) ambayo ni ya nchani mwa marando (mche) na kubakiza  ncha ili mti uendelee kuota. Majani hayo huchukuliwa na kuvurugwa vurugwa kwa mkono mpaka ile rangi ya kijani  kibichi kugeuka na kuwa kama ya ukahawia au kuwa nyeusi nyeusi kisha huanikwa majani hayo juani kidogo, halafu huchemshwa kwa muda kama wa dakika 40 hivi. Hutiwa viungo kama vile chumvi kwa ajili ya ladha, lakini mpishi asisahau kutia Ntwili,  ambazo ni karanga zilizo kaangwa na kusagwa na kupatikana tui la karanga.  Mboga hiyo  ama  inawezakutumika kama kitoweo cha ugali wa muhogo au wa mahindi  au kumwagiliwa kwenye wali wa maji, chakula chenye mvuto mkali.
Ama aina ya pili ya kutengeneza matembele ni kuwa yakisha kuchumwa  husuguliwa na kunyaushwa kama yale mengine ya matumizi ya mara moja, lakini hukaushwa kwa muda mrefu juani na kisha huwekwa ndani ya hazina  ambayo kwa Wanyamwezi hukoboa gome la mti na kutengeneza kilindo ambacho huwa na umbo la mviringo. Matembele hayo huweza kukaa hata mwaka  yakisubiri wakati watu wana shida ya kupata kitoweo. 

Inakuwa ni rahisi kutumia au kama mgeni kutokea saa ambazo ni mbovu kupata kitoweo, basi anatayarishiwa chakula na hicho ndio kitoweo chake. Matembele yaliyo kaushwa watu wa siku hizi wanayaita rasta kwa kufanana kwake na nywele za rasta.

Matembele huweza kutumika kwa kuchanganywa na nyama ya mbuzi ambyo ilibanikwa 
na kuwa kavu vikipikwa pamoja, hapo mambo yanakuwa si mchezo, watoto hawachezi mbali. Pia huweza kupikwa pamoja na samaki waliokaushwa kwa moshi, lakini siyo kambare na pia matembele yanakwenda sawia na dagaa wa Kigoma kwa mafuta ya mawese.
Na majani ya viazi yakikauka huwa ni chakula kizuri sana kwa wanyama kama vile ng’ombe na mbuzi.
Ama mizizi ya mmea huo, mimi siiti kama ni mizizi, kwa ufahamu wangu ni kuwa mzizi hutumika kupitishia maji na chakula cha mmea kwenda kwenye shina, na mizizi hutumika kufanya mmea kuwa imara aridhini ili using’olewe na ama wanyama au upepo au mvua yenye upepo na hivyo huwa imekomaa na ni miti mikavu . Sasa mmea huu, mizizi yake ni tofauti na hayo, mizizi yake ni laini sana na huvimba kwa sababu hutumika kwa kuhifadhia chakula, na sijui kama chakula hicho ni kwa ajili ya mmea huo, bali hiyo ni neema tu tuipokee tuwaachie wataalamu wa mimea watafanya uchambuzi wenyewe.
Mzizi wa matembele  huitwa kiazi na kiazi kina sifa nyingi sana  tukiachilia mbali hali ya kuwa ni kitamu na Waswahili waliona watoe jina la ufafanuzi na kuuita mzizi huo kuwa ni Kiazi kitamu.
Pengine kwa sababu ya utamu wake  ndiyo kilicho wafanya Wanyamwezi wasiache kupanda hata shina moja kwenye kishamba kidogo. Ukimuliza atakwambia kuwa hiyo ni mbegu.
Na viazi hutumika kwa namna nyingi kama ifuatavyo:

1.     Kutafunwa kiazi mara tu kinapokuwa kimetolewa ardhini, ni mzizi mtamu wa ajabu, muhogo haufui dafu.
2.     Kiazi huweza kuchukuliwa na kuokwa na kikiwa tayari basi kinakuwa ndani kimeachana na kinashikiliwa na gamba lake la juu tu. Hapo ladha yake siwezi kuieleza kwa sababu ulaji wa kiazi kilichookwa kwenye majivu ya moto huweza kupotea sehemu kubwa kwa kuwa ule unga unga unamwagika ingawa unakuwa bado kuna unyevu unyevu.
3.     Kuchemshwa kama muhogo na kuiva hali yake inakuwa karibu na kile kiazi kilicho okwa kwenye majivu ya moto. Sasa maajabu ni kuwa kiazi ni kitamu lakini kikichemswa basi kitumie kula kwa kutowelea kwa asali. Ndiyo Asali tamu na Kiazi Kitamu. Jaribu utaona!

KIAZI KAMA AKIBA YA SIKU ZA UHABA WA CHAKULA.

Ama kwa matumizi ya viazi kama tulipotaja hapo juu ni jambo la kawaida na huweza kupatikana katika makabila mengi ambayo hutumia viazi vitamu, lakini Wanyawezi wamepata umarufu kwa viazi kwa kula viazi kwa asali na pia kuweza kuvihifadhi viazi kwa nyakati za uhaba wa chakula na wamekuwa wakitumia njia zifuatazo: 
  (a)    Matununtwa: Viazi vikiwa  ni vidogo vidogo pengine ukubwa wa  dole gumba, hivyo havitupwi kwa sababu huo ni ubadhirifu. Badala yake huchukuliwa hivyo na kunyaushwa juani nasisitiza kunyaushwa na sio kukaushwa. Halafu utayarishaji unaendelea kwa kuchukuliwa hivyo vifaranga vya viazi vilivyo nyauka na kupondwa kidogo tu kwa kutumia nyundo ya mti (mallet) na bila kusambaratishwa huanikwa  ama kwenye jamvi, au mkeka au kwenye mwamba wa mawe ulio tambarare (matare). Viazi hivyo vikihakikishwa kuwa vimepoteza unyevu unyevu ni vikavu kukutu huchukuliwa na kutiwa ndani ya hazina – hasa kilindo. Hii hazinayetu huitwa matununtwa 
  (b)   Makewe: (slesi)  Huchukuliwa viazi vya kipimo vya kawaida ambavyo uzito wake kama  gramu 250 na mara vikitoka shambani kwa sababu viko vingi, vinatakiwa kuhifadhiwa kwa ajili ya  matumizi ya baadaye. Hivyo huchukuliwa visu vya kawaida  ambavyo si vikali sana  na  viazi hivyo huchaangwa kwa urefu, vikapatikana kama vipande bapa vitano sita au saba kutoka kila kiazi. Vipande hivyo huanikwa mpaka unyevu wake kuisha halafu huwekwa kwenye hazina. Kama ni vichache huwekwa kwenye kilindo au lindo kubwa. Na kama ni ghala kubwa basi huchukuliwa majani ya mpunga yaliyokauka na kutandikwa na kuwekwa hayo Makewe. Hapo viazi hivyo vikiwa 
katika hali hiyo vinawezakukaa zaidi ya mwaka na kisha vikatumika bila matatizo. 
    (c)    Matobolwa: Viazi vinapokuwa katika hali ya wingi, mara baada ya kutoka shambani huchukuliwa na kunyaushwa juani kidogo na kupoteza baadhi ya unyevu wake. Mtu akivishika anaona kama vile vinabonyea kwa kupoteza  unyevu wake. Hapo viazi vinakuwa viko tayari kutengeneza matobolwa kwa hatua zifuatazo:
(i)                Hutengenezwa makebwe kama hapo juu kifungu cha (b)
(ii)             Pili huchukuliwa makebwe hayo na kuchemshwa kwa muda mfupi kwa maji kidogo sana  ili kupata mvuke ambao utatumika kuivisha slesi hizo za viazi.
(iii)           Vikiiva bila kusamabaratika huipuliwa kutoka jikoni.
(iv)           Kisha huopolewa kutoka mule vilimo pikiwa
(v)              Na kwenda kukaushwa kwa jua kali
(vi)           Hapo viko tayari kuwekwa kama akiba ya chakula.
 Neno matobolwa ndilo linatajwa kuwa ndio asili ya mji wa Tabora, kwa kuwa Wanyamwezi wao wana lugha ambayo haina herufi Ra na wingi wa mambo huongeza kwa kutia Ma nyuma ya neno, watu waliokuja hapo walimkuta Bibi kizee  akianika matobolwa yake  akaulizwa  nini hicho? Alijibu, Matobolwa .  Walichuka neno hilo na kulitohoa au kulihariri na kuiita mahali hapo ni TABORA.





[1] Angalia kitabu cha Mzee David Yongolo, Bara Unyamwezi/Wanyamwezi


SENENE  WA MAAJABU KATIKA MAJUMBA YA WATU

SENENE KAMA WANAVYOONEKANA KATIKA PICHA








































































Senene  kwa Kihaya "Ensenene", ni aina ya panzi wenye rangi ya ambao  hupatikana sana  wakati wa  masika katika maeneno mbali nchini kwetu. Lakini huko Kagera wanapatikana katika musimu wa miezi ya Novemba na Desemba. Wanaweza kuitwa kwa majina mengine  mengi, lakini kwa Kiingereza wanaitwa Grasshoppers maana yake ni    panzi!  Senene wanaliwa na watu kwa namna yoyote ile kama chakula au mboga, napengine kama kiburudisho. Kuna maeneo kadhaa ambako senene hutumika kama kifungua kinywa kabla chakula kikuu hakijawa tayari lakini kwa ujumla ni watu wengi wanapoanza kutumia senene kama kitoweo huuma chanda na kujuta kwa nini walichelewe kula senene! Hiki ni kitoweo chenye protini nyingi na kimetulia mdomoni. Watu wengine wanawafafanisha senene na uduvi,  ah  si mlinganisho sahihi maana senene huna haja ya kunawa kwa sabuni eti unaondoa shombo… hilo halipo. Watu wengi wanapenda kuwala hawa senene kwa sababu ya ladha tu wengine kwa sababu za kukamilisha mlo  na wengine wanasema kuwa  husaidia kuleta utulivu na kujenga heshima ndani ya nyumba. Hapo zamani kitoweo hiki kilihusishwa na kabila la Wahaya lakini kwa sasa watanzania walio wengi wanakula. Ni ambacho kinatumika katika mikoa mingi ya nchini Tanzania.
 Lakini senene wakiwa ni wengi huweza kushambulia mashamba ya mahindi au mtama au uwele na kuleta madhara ya njaa kubwa katika jamii na mwaka huo huitwa  MWAKA WA SENENE, ingawa madhara yake hayafikii yale ya panzi aitwaye NZIGE..


Senene "Ensenene" Kwa kihaya, inaweza kuitwa kwa vyovyote vile ama chakula, mboga, au kitafunwa, ni moja ya baraka kubwa ambayo haijawaikutokea kwa kupata kitoweo kama hiki chenye protini kubwa. Wengine ukihusianisha na uwezo wake mkubwa wa kuimarisa ndoa. Hapo zamani kitoweo hiki kilihusishwa na wahaya lakini kwa sasa watanzania walio wengi wanakula. na pia kitoweo hiki kwa sasa kinapatikana mikoa mingi. "Kula senene linda ndoa"


VITUNGUU, KIUNGO CHA CHAKULA CHENYE FAIDA KWA MKULIMA

Na Mjomba Remsi 




Hapo awali kitungu kilikuwa ni zao lililokuwa linapatikana porini katika ukanda wa bahari ya Mediterania. Zao hili hulimwa katika nchi nyingi za magharibi, nchi za milima zilipo kaskazini mwa dunia, likwemo bara la Afrika. Vitunguu hustawi katika hali ya hewa ya jotoridi 13°C – 24°C, hali ya hewa inayofaa kwa kuotesha na kukuzia miche kwenye kitalu ni jotoridi 20°C – 25°C. Kwa kawaida vitunguu huhitaji kiasi cha joto nyuzi 20°C-25°C ili kuweza kustawi na kukua vizuri. Joto zaidi ya hapo hufanya vitunguu kudumaa na kutoweza kutengeneza viazi (bulbs).

MATUMIZI 


Kitunguu hutumika kama kiungo cha kuongeza ladha kwenye chakula, na pia hutumika kama dawa ya kansa ya tumbo, vidonda na majipu.
USTAWI
    
Zao la vitunguu hustawi katika udongo wa tifu tifu wenye mbolea ya kutosha, ukiwa na uchachu wa udongo (PH) kiasi cha 6 – 6.8.  Udongo wa mfinyanzi haufai kwa zao la vitunguu kwa kuwa hauruhusu viazi vya vitunguu (bulbs) kutanuka.  Hivyo uwezekano wa kupata mazao ni mdogo. Pia udongo wa kichanga haufai kwa zao la kitunguu kwa kuwa hauna mbolea na hivyo vitunguu huwa vidogo sana, jambo ambalo ni vigumu kupata mazao yanayofaa kwa soko.

Zao la kitunguu huhitaji unyevu muda wote wa ukuaji wake. Zao hili lina mizizi mifupi hivyo linahitaji kumwagiliwa maji mara kwa mara.



AINA ZA VITUNGUU MAJI

Kuna aina mbili za vitunguu ambazo zimezoeleka:
• Vitunguu maji vile vinavyopatikana sana Singida, na Rujewa (aina hii ina rangi ya kahawia iliyopauka) na majani yake ni mabomba ya kijani.
• Chotara: Hii ni aina ya vitunguu inayojulikana kama vitunguu vya kisasa. Katika kundi hili kuna vitunguu kama Texas grano, Red creole, Bombay red, White granex, na Super rex.

MGAWANYIKO 

Zao la vitunguu limegawanyika katika makundi mawili. Hii inatokana na uhitaji wa mwanga na ukuaji wake. Aina ya kwanza inahitaji mwanga kwa saa 8-13 kwa siku ili kuweza kuchanua na kutoa mbegu.

Aina ya pili inahitaji mwanga kwa saa13-15 kuweza kuchanua na kutoa mbegu.

KUPANDA 
Vitunguu hupandwa kwa kutumia mbegu ambazo husiwa kwenye vitalu.  Kitalu kinaweza kuwa na upana wa mita 1, urefu unategemeana na ukubwa wa eneo alilo nalo mkulima.

Unaweza kupanda vitunguu kwenye matuta mbonyeo (Sunken bed). Aina hii ya upandaji hutumika kwenye eneo lenye shida ya maji. Upana wa tuta uwe mita moja.

Au ukapanda kwenye matuta mwinuko (Raised bed) upandaji wa aina hii hutumika sehemu yenye maji meng iau yanayotuama.
TAHADHARI 

Maji yakituama kwenye vitunguu hufanya vitunguu kuoza, hivyo kuathiri mavuno.

NAFASI

Vitunguu vipandwe kwa nafasi ya sentimita 7.5 kutoka mche hadi mwingine., na  sentimita12.5 kutoka mstari mmoja hadi mwingine kwenye matuta.

MBOLEA YA KUPANDIA 

Unaweza kutumia mboji, au samadi iliyo oza vizuri kupandia. Baada ya hapo unaweza kuongeza mboji baada ya miezi miwili. Endapo unafanya kilimo kisichozingatia misingi ya kilimo hai, unaweza kupanda kwa kutumia mbolea aina ya NPK (20:10:10) baada ya mwezi na nusu, unaweka mbolea ya Urea.

PALIZI 

Vitunguu ni zao lenye uwezo mdogo sana wa kushindana na magugu. Hivyo, inabidi shamba liwe safi muda wote wa ukuaji hadi kuvuna.

UVUNAJI

Kwa kawaida, vitunguu huchukua muda wa miezi 5-6 tangu kupandwa hadi kuvunwa. Unaweza kuanza kuvuna vitunguu baada ya asilimia 75 ya shingo za vitunguu kuvunjika.  Baada ya kuvuna, unaweza kuweka kwenye madaraja (grades) kwa kufuata ukubwa, rangi na unene wa shingo ya kitunguu. Vitunguu vyenye shingo nyembamba hudumu zaidi, vyenye shingo nene huoza haraka.

UKATAJI 
Hakikisha kuwa shingo ya kitunguu inabaki kiasi cha sentimita 2. Hii husaidia kuzuia kuoza kwa zao hili haraka.

NAMNA YA KUHIFADHI VITUNGUU 
Baada ya kuvuna, hifadhi vitunguu kwenye kichanja chini ya kivuli na uvitandaze vizuri. Unaweza pia kuhifadhi vitunguu kwa kuvifunga kwenye mafungu na kuvitundika.  Vitunguu vikihifadhiwa vizuri vinaweza kukaa hadi miezi minne bila kuharibika, hii hutegemeana na aina ya uhifadhi.
WADUDU WANAOSHAMBULIA VITUNGUU 
Kuna aina nyingi za wadudu wanaoweza kushambulia vitunguu.  Hawa wafuatao ni baadhi ya wadudu waliozoeleka kwenye zao la vitunguu.
                             
THIRIPI

Thiripi (Thrips): Wadudu hawa hukaa kwenye jani sehemu inayokutana na shina. Wadudu hawa hufyonza maji kwenye majani ya vitunguu na kusababisha majani kuwa na doti nyeupe.
Madhara: Husababisha vitunguu kudumaa hivyo kuathiri ukuaji wake jambo ambalo huathiri mavuno pia.           

                                                    KIMAMBA
Kimamba: Wadudu hawa hufyonza maji kwenye vitunguu, na kusambaza ugonjwa wa virusi. Husababisha kudumaa kwa vitunguu. Wadudu hawa ni hatari zaidi kwa kuwa husambaza virusi vinavyoingia hadi kwenye mbegu.

Minyoo fundo (Nematodes): Aina hii ya minyoo hushambulia mizizi ya vitunguu. Hali hii husababisha kudumaa kwa vitunguu kwa kuwa hushindwa kufyonza maji na chakula kutoka ardhini.

Vidomozi (Leaf minor): Hushambulia majani kwa kujipenyeza kwenye ngozi ya jani na kusababisha michoro ambayo huathiri utendaji wa majani.

Utitiri mwekundu (Red spider mites): Wadudu hawa hufyonza maji kwenye majani na kusababisha vitunguu kunyauka.

Funza wakatao miche: Funza hawa hutokana na wadudu wajulikanao kama Nondo, na hushambulia shina na kulikata kabisa.



NAMNA YA KUKABILIANA NA WADUDU HAWA

Unaweza kukabiliana na wadudu hawa kwa kufanya kilimo cha mzunguko.  Usioteshe vitunguu sehemu moja kwa muda mrefu, au kufuatanisha mazao jamii ya vitunguu kama vile leaks.

Tumia mbegu bora zilizothibitishwa kutoka kwenye kampuni zinatambuliwa kisheria na kibiashara.  Kupanda kwa wakati unaotakiwa; vitunguu visipandwe wakati wa kiangazi. Vipandwe wakati wa majira ya baridi na kuvunwa wakati wa joto. Tumia dawa za asili za kuulia wadudu, au dawa nyinginezo zinazopendekezwa na wataalamu wa kilimo.

                         MAGONJWA YANAYOSHAMBULIA VITUNGUU
                           
PURPLE BLOTCH

1. Purple blotch: Ugonjwa huu husababishwa na ukungu (fungus). Ugonjwa huu husababisha mabaka ya zambarau na meusi katika majani ya vitunguu.  Ugonjwa huu hutokea wakati wa unyevu unyevu mwingi.
Madhara: Ugonjwa huu hupunguza mavuno mpaka asilimia hamsini (50%).

2. Stemphylium leaf blight: Hukausha majani kuanzia kwenye ncha hadio kwenye shina.; Ugonjwa huu hutokea wakati wa unyevu na ukungu mwingi.
Madhara: Hupunguza mavuno hadi kwa asilimia sabini na tano (75%).
UNION YELLOW DRAFTS VIRUS

3. Magonjwa ya virusi (Onion yellow draft virus): Ugonjwa huu husababisha vitunguu kuwa na rangi iliyochanganyika, kijani na michirizi myeupe au njano.  Vitunguu hudumaa kwa kiasi kikubwa;Ugonjwa huu husababishwa na kimamba.
Madhara: Huathiri mavuno kwa asilimia 80 mpaka asilimia 100%.
4. Kuoza kwa kiazi (Bulb rot): Husababishwa na fangasi. Ugonjwa huu hutokea vitunguu vikishakomaa, huku udongo ukiwa na maji maji.  Vitunguu vikishakomaa visimwagiliwe tena.

UHARIBIFU WA VITUNGUU USIOTOKANA NA MAGONJWA 

1. Kuchipua baada ya kuvunwa: Hali hii hutokea endapo:
1.      vitunguu vitavunwa kabla ya muda wake. 
2.     Endapo vitunguu havitakaushwa vizuri baada ya kuvunwa.
Hali hii husababisha uharibifu mpaka asilimia themanini (80%).  Sehemu ya kukaushia vitunguu iwe na hewa inayozunguka na mwanga wa kutosha. Vitunguu vikiwekwa gizani huchipua kwa urahisi.
 
2. Muozo laini (Soft rot): Ugonjwa huu hushambulia vitunguu baada ya kukomaa; husababishwa na vimelea (bacteria). Vitunguu hutoa harufu mbaya ya uozo.  Kuepuka hilo vuna kwa wakati unaofaa, hifadhi sehemu yenye mwanga na hewa inayozunguka.

Virusi
Unaweza kuzuia vimamba ambao ndio wanaoeneza virusi kwa kutumia dawa za kuulia wadudu


VITUNGUU VINALIPA 

Peniel Rodrick Mkulima wa Vitunguu

“Vitunguu vinatofauti kidogo na mazao mengine ya mboga mboga kwa kuwa si rahisi kukosa soko, na endapo bei si nzuri unaweza kuvihifadhi kwa muda ili kusubiri bei iwe nzuri.” Ni maneno ya mkulima Peniel Rodrick (pichani) ambaye amejikita zaidi katika kilimo cha vitunguu kibiashara.  Mkulima huyu kutoka kijiji cha Oloigeruno anasema pamoja na kwamba anazalisha pia mazao mengine, lakini ameamua kujikita zaidi kwenye vitunguu baada ya kugundua siri na namna ya kupata faida zaidi.

Toka aanze kilimo cha vitunguu miaka 12 iliyopita, ameweza kuendesha maisha yake vizuri, ikiwa ni pamoja na kuanzisha miradi mingine kama ufugaji wa ng’ombe, kujenga nyumba ya kisasa na kuitunza familia yake ya watoto watatu ipasavyo. Pamoja na hayo anasema tatizo kubwa la vitunguu ni magonjwa na wadudu. Anasema si rahisi sana kugundua mara moja kuwa kuna ugonjwa unaoshambulia vitunguu, na mara unapogundua unakuwa umefikia kwenye hali mbaya.
                                               VITUNGUU 

Na Mjomba Remsi,

Ndugu Bunyanza  akiwa anaona kuwa kula mshikaki kwa kachumbari anauliza hivi vitu gani na vinatoka wapi. 

Kachumbari ina vifaa vingi lakini hapa tunazungmzia juu ya VITUNGUU kwanza. Sisi bila hiyana tunawelezea yale machache tuliyo nayo.





Zao la vitunguu hulimwa karibu kila mahali hapa nchini. Hata hivyo, mikoa inayolima kwa wingi ni Tanga, Arusha, Iringa, Kilimanjaro, Singida, Morogoro, Mara, Mbeya Dodoma na Manyara.

Zao hili ni la biashara na chakula. Ekari moja inaweza kuzalisha gunia 80 – 100 za vitunguu zikitunzwa kitaalam, na mkulima anaweza kulima mara mbili kwa Mwaka kwa mbegu kubwa ambazo huchukua hadi miezi mitano (5) shambani. Bei ya wastani kwa gunia moja ni Tsh 60,000

MAMBO YA KUZINGATIA WAKATI WA UZALISHAJI 

Ili kupata vitunguu bora na vingi ni muhimu kuzingatia kanuni za kilimo bora cha vitunguu.Baadhi ya kanuni hizo ni kama zifuatazo: -

                              

VITUNGUU VIKIWA SOKONI TAYARI KWA KUUZWA

1 - Kuchagua aina ya mbegu

• Chagua aina bora kulingana na matakwa ya soko
• Pamoja na mahitaji ya soko ni muhimu pia kuchagua aina inayovumilia magonjwa, wadudu na hukomaa mapema na kutoa mazao mengi na bora.

2 - Kuweka mbolea
Vitunguu hustawi vizuri kwenye udongo wenye rutuba ya kutosha.
• Tumia mbolea za asili ili kurutubisha udongo kwa lengo la kupata mazao mengi na bora.
• Iwapo ni lazima kutumia mbolea za viwandani muone mtaalam wa kilimo ili akuelekeze namna ya kutumia. Mbolea ikizidi huharibu ubora wa vitunguu.

3 - Kumwagilia maji
• Kagua shamba kuona kama udongo una unyevu wa kutosha. Iwapo unyevu ni mdogo mwagilia maji kufuata mahitaji ya mmea. Vitunguu vinapoanza kukomaa punguza kumwagilia ili kuepuka kuoza

4 - Kupalilia
• Palilia mara kwa mara ili kudhibiti magugu na kuwezesha vitunguu kutumia vizuri unyevu na virutubishi vilivyoko kwenye udongo. Pia magugu mengine huficha wadudu waharibifu kama vile utitiri mwekundu.
• Wakati wa kupalilia epuka kukata mizizi ya mimea.
• Pandishia udongo na kufunika shina la kitunguu wakati wa kupalilia ili kuzuia jua lisiunguze mizizi na kubabua vitunguu. Vitunguu vilivyoungua na kubabuliwa ubora wake hushuka napia huharibika upesi wakati wa kuhifadhi.

5 - Kudhibiti magonjwa na wadudu
Vitunguu hushambuliwa na magonjwa na wadudu mbalimbali ambao huweza kusababisha upungufu na ubora wa mazao. Ili kudhibiti tatizo hilo kagua shamba mara kwa mara kuona dalili za mashambulizi. Endapo kuna dalili za mashambulizi, chukua tahadhari ya kunyunyuzia dawa mapema kabla madhara hayajaleta upotevu mkubwa.

6 - Kupanda kwa nafasi:
Zingatia nafasi ya kupanda inayopendekezwa ili kupata vitunguu vyenye ukubwa uliokusudiwa. Wastani ni inchi 4 - 5 kutoka kitunguu kimoja hadi kingine, na inchi 12 - 18 kutoka mstari hadi mstari na kipandwe inchi 1 - 1.5 chini ya udongo


                             MAANDALIZI KABLA YA KUVUNA

1 - Kukagua shamba
• Kagua shamba ili kuhakikisha kuwa vitunguu vimekomaa. Vitunguu huwa tayari kuvunwa miezi mitatu hadi mitano tangu kusia mbegu kutegemea aina ya mbegu na hali ya hewa.Dalili za vitunguu vilivyokomaa:

• Majani hunyauka na kuanza kukauka
• Asilimia kumi hadi 20 ya mimea huanguka majani na shingo hulegea.
• Majani hubadilika rangi kuwa ya manjano na baadaye kaki


                          
VITUNGUU VILIVYOKAUKA MAJANI 
TAYARI KWA KUVUNA


2 - Kuvuna
Vitunguu vinapaswa kuvunwa mapema mara tu vinapokomaa ili kupata mazao mengi na bora.Uvunaji hufanyika kwa mikono ambapo jembe uma hutumika kuchimbua au kulainisha udongo.Udongo ukishalainishwa vitunguu hung’olewa kwa mkono. Inashauriwa uvunaji uanze asubuhi ili vitunguu viweze kunyauka na kukomaza ngozi sehemu za michubuko. Vitunguu visiwekwe juani na inapobidi kukomaza ngozi shambani, majani ya vitunguu yatumike kufunika vitunguu ndani ya matuta yake wakati wa mchana ambapo kuna jua. Kusanya vitunguu kwenye vikapu kisha vipeleke sehemu ya kukaushia. Vitunguu vya vikianikwa kwenye kichanja ni bora zaidi, mizizi na majani hupunguzwa na kuachwa urefu wa robo inchi . Vitunguu vya kukausha kwa kunining’iniza havikatwi majani bali hufungwa kwenye mafungu na kupelekwa sehemu ya kukaushia.



MAMBO YA KUANGALIA MENGINE  JUU YA VITUNGUU:

·        Watu wa Yemeni na vitunguu
·        Watu waonaishi majangwani wanakula sana vitunguu.
·        Malori ya vitunguu hupatikana kwa wingi wakati wa Hijja huko Makkah
·        Wazungu wanapenda sana Vitunguu maji kwa sababu vinakazi nyingi mwilini.













 










                   


              

                   



           


                         
   
      








 





No comments:

Post a Comment