Wednesday, September 7, 2016

MAALIM SEFU NA PROFESA LIPUMBA  (WOTE WALIMU KWA KIARABU NA KIFARANSA)


Hali ya chama cha wananchi (CUF) kuwa katika hali isiyoeleweka kunatia  wasi wasi juu ya uimara wa chama hicho kikiwa kama miongoni mwa vyama Vya upinzania vyenye nguvu nchini Tanzania.

Wadadisi wa siasa  wanaona kama vile chama hicho sasa kimo katika mgawanyiko mkubwa , kwa sababu uongozi wa juu haujakaa vizuri. Kila mwalimu na mwelekeo wake, Maalim Sefu ana mambo yake na Profesa Lipumba anasema hayakubali anayoyasema Maalimu Sefu.
Profesa Lipumba  anasema yeye ni ngangari kinoma  na ni bado mwenyekiti wa CUF licha ya kuwa alisikia vyombo vya habari vikitangaza kuwa katibu mkuu Maalim seif amemwondoa katika uenyekiti.

Na Katibu Mkuu, Maalim Seif anaonekana naye yuko imara katika kutaka kumng’oa Profesa katika nafasi hiyo.Kamweka Mtatiro kuwa Mwenyekiti, mtu ambaye ni bingwa wa sheria kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Chanzo ni kuwa wakati wa uchaguzi mkuu mwaka jana (2015) baada ya Edward Lowassa kutemwa na Chama cha Mapinduzi, alitaka mahali pa kujibana ili apate fursa ya kugombea. 

(Inasemekana) alikwenda katika vyama vingi, na alipokwenda kwa Profesa alishauriwa aende Chama Cha Demokrasia  (CHADEMA).
Wanasema kuwa Lowassa alitaka kuingia CUF, swali likawa nani atakuwa mgombea na nani mgombea mwenza?  Kwa katiba ya CUF Lowassa hakuweza kuingia mara moja na kuanza kugombea nafasi ya kitaifa mara moja kabla hajakaa katika chama cha Wananchi kwa muda wa miezi sita (6) kwa mujibu wa Katiba.

Lakini kwa Lowassa peke yake  kuwa huko CHADEMA ilionekana kuwa hawezi kupata kura za Waislamu ambao ni kundi  kubwa  nchini licha ya kujaribu kwake kuwekeza kwa kutoa misaada ya kuwasaidia sehemu mbali mbali pamoja na kutoa misaada katika misikiti kadhaa. 

Hivyo, ili kufikia hatua ambayo ingelimweka pazuri na aone yuko vema ni kumpata Maalim Juma Duni wa CUF aingie CHADEMA kama mgombea mwenza kwa ajili ya kupata kura za Waislamu. 

Kilichomfanya Lowassa akose kupata kura hizo ni kauli ya Mchungaji ambaye alikuwa mshauri wake wa mambo ya dini huko katika kampeni  alipotangaza kuwa Lowassa akitawala, basi misikiti yote nchini baada ya siku mia moja itageuka na kuwa  “nursery schools”

Ilikuwa rahisi kwa Lowassa kuingia CHADEMA , kwanza kama home boy na nadhani katiba ya chama hicho haina vikwazo kama vya CUF, ndiyo maana Mwalimu Juma Duni aliweza kuingaia pampja na Lowassa na wote wawili wakafanya kazi kama majeshi ya kukodi ya CHADEMA. Na mara tu baada ya uchaguzi na kukosa  kilichokuwa kinakusudiwa mgombea mwenza alirejea zizini CUF.

CUF isingelifanya uchaguzi wa ndani mara baada ya uchaguzi maana Juma Duni ambaye alikuwa anaaminika kuwa angelikuwa Mwenyekiti baada ya Profesa kujiuzulu uenyekiti kabla hajafikisha miezi sita kulingana na katiba. Na mkutano ulioandaliwa hapa Dar es Salaam inasemekna ilikuwa kama kiini macho  maana uliandaliwa visiwani lakini watu wa Bara hawakukaribishwa. Kwa kawaida Visiwani wajumbe wake huwa ni wachache kuliko wajumbe wa Bara lakini  wajumbe wa Visiwani safari hii walikuja wengi zaidi ya wajumbe wa bara na wajumbe wengine wa  Bara anasema Profesa hawakuwa na habari ya kikao hicho akiwemo yeye.

Anasema kweli aliomba kujiuzulu uenyekiti kabla ya Uchaguzi Mkuu mwaka 2015, lakini alitengua hilo kwa barua yake nyingine na kwa hali hiyo yeye anasema ni Mwenyekiti wa CUF na Msajili wa Vyama  nchini analijua hilo.

Asilokubali  Lipumba ni kuwa ametangazwa kuwa si Mwenyekiti kwenye vyombo vya habari , lakini hajaambiwa rasmi ama kwa simu au kwa barua. Aletewe barua ili aone kimesema nini na tuhuma zake ni zipi. Anasema mchezo unaofanyika ni kuwa wanataka siku 14 zipite ili asipate fursa ya kufanya rufaa.

Sasa, watu wanasema CUF ni chama cha nani na cha wapi? Kama cha Visiwani alikianzisha nani?  Na kama cha Bara Mapalala yuko wapi?   Kikimeguka kuna faida gani itatokea?

Habari za mbali zinaeleza kuwa Maalim Seif na Profesa Lipumba walikuwa pamoja katika moja ya taasisi za kielimu hapa nchini katika udogo wao, na inasemekana wanajuana fika: “Wakiwa kwenye jukwa la siasa wanakaa kama Mr Chairman and Secretary General, lakini wakiwa nje haisemeki hao watu walivyo karibu. Wanakumbatiana na kuleta jokes  za miaka ya 1970s huko masomoni kwao.
Mwisho/

No comments:

Post a Comment